"Tunaomba radhi, hatukupenda" - kocha Taifa Stars

Jumatatu , 23rd Sep , 2019

Kaimu kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Juma Mgunda amewaomba radhi mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla baada ya kupoteza mchezo wa nyumbani jana dhidi ya Sudan.

Mchezo wa Taifa Stars na Sudan katika Uwanja wa Taifa

Katika mchezo huo wa kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani 'CHAN' uliofanyika jana katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam, Taifa Stars imefungwa bao 1-0, bao la Sudan likifungwa katika dakika ya 61 na Yassir.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha Juma Mgunda amesema kuwa wanafahamu Watanzania wanahitaji furaha na walikuwa na mategemeo makubwa katika mchezo huo lakini mpira una matokeo tofauti.

"Nichukue nafasi hii kuwatakeni radhi Watanzania wote kwa ujumla kutokana na matokeo tuliyoyapata, hii ni sehemu ya mchezo na tumeona kilichotokea, tulijitahidi kutafuta ushindi lakini haikuwa hivyo", amesema.

"Kila mmoja ameona mchezo tulivyocheza, tutakwenda kufanyia kazi mapungufu yaliyotokea. Nirudie tena kuwaomba radhi, hatukupenda kuwaudhi lakini muendelee kutuombea, msichoke", ameongeza Mgunda.

Mchezo wa marudiano unatarajia kupigwa Oktoba 18, 2019 katika uwanja ambao si wa nchi ya Sudan kutokana na hali ya nchi hiyo kutokuwa sawa.