Jumamosi , 16th Jun , 2018

Nahodha wa Mabingwa watetezi wa michuano ya Kikapu Sprite Bball Kings, Mchenga Bball Star Mohamed Yusuf, amesema wamekuja kusajili timu yao kwa lengo la kutetea ubingwa wao na hakuna timu itawasumbua.

Mohamed ameyasema hayo mchana huu kwenye usajilili wa timu shiriki za mwaka 2018, unaoendelea hapa Mlimani City Mall ambapo ameahidi kuwa msimu huu wamejipanga zaidi kuliko msimu uliopita.

''Nachoweza kusema tu kuwa timu zinazojiandikisha zijue kuwa zina kazi ya kupita kwenye mchujo kwanza kabla ya kutufikia sisi kwenye hatua ya 16 bora, hivyo wajue sisi tupo tunawasubiri na hakuna timu itakayochukua kombe letu'', amesema.

Mbali na hayo Mohamed ameipongeza East Africa Televison na Kampuni ya Cocacola kupitia kinywaji cha Sprite kwa kuendelea kuwekeza kwenye mchezo wa Kikapu na kuinua vipaji vya vijana wengi.

Timu zaidi ya 30 tayari zimeshajisajili kwaajili ya michuano ya mwaka huu ambapo bingwa atakuwa anawania kiasi cha shilingi milioni 10 pamoja na Kombe, huku mshindi wa pili akiwania milioni 3 na MVP atajitwalia milioni 2.