Jumanne , 2nd Feb , 2021

Kocha msaidizi wa klabu ya soka ya Tanzania Prisons Shaban Kazumba maarufu kama Mourinho amesema baada ya maboresho ya kikosi katka dirisha dogo la usajili, kwa sasa wanawania ubingwa.

kikosi cha Tanzania Prisons chini ya Salum Mayanga na Shaban Kazumba' Mourinho' kimejinasibu kutwaa ubingwa wa VPL msimu huu

Amesema ''tumesajili wachezaji wapya wa 4 katika dirisha hili dogo,wenye uwezo wa hali ya juu na ambao timu iliwakosa katika duru la kwanza, tunaamini sasa tunaweza kabisa kuwania ubingwa mara baada ya kupata saini hizi zitakazoongeza ubora katika timu yetu''.

Katika dirisha hili la usajili klabu ya soka ya Tanzania Prisons imefanikiwa kuwasajili wachezaji wanne akiwemo mshambuliaji Stamili Mbonde toka Mtibwa Sugar, mlinzi Kennedy Kipepe toka Coastal Union, Kiungo wa pembeni Seleman Mangoma toka Mbeya City na Shaban lyamu kutoka Lipuli.

Prisons inatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki mkoani Mbeya, moja ukiwa umeshathibitishwa dhidi ya Ihefu, na nyingine wanatarajia kucheza na timu za daraja la kwanza na Boma toka Kyela, kabla ya kikosi chao kurejea Sumbawanga kucheza mchezo wa ligi dhidi KMC tarehe 13/2/2021.

Tanzania Prisons ipo kwenye nafasi ya 9 kwenye msimamo wenye jumla ya timu 18, ikiwa na alama 22 ikiwa imeshuka dimbani mara 18, katika michezo 16 iliyobaki ili kumaliza msimu, michezo 8 ni ya nyumbani na 8 iliyobaki ni ya ugenini.