Utata wa Kakolanya wamalizwa

Jumanne , 14th Mei , 2019

Aliyewahi kuwa mlinda mlango namba moja wa klabu ya Yanga msimu huu, Beno Kakolanya, hatimaye amekuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kuvunjika.

Beno Kakolanya

Kakolanya ambaye kwa muda mrefu amekuwa nje ya uwanja kutokana na kutofautiana na kocha wake Mwinyi Zahera, kwa sasa yupo huru kujiunga na timu yoyote baada ya mkataba wake na Yanga kuvunjwa.

"Mimi sijafuatwa nisiwe muongo, naona tu kwenye vyombo vya habari watu wanaandika kunihusisha na Simba, Yanga na Azam lakini ofa ni nyingi alizonazo meneja wangu." - Amesema Beno.

Kuhusu kurejea tena Yanga Beno, amesema mpira ndio kazi yake hivyo hawezi kusema hatamani kurudi mahali kwakuwa yeye ni mchezaji hivyo anaweza kucheza sehemu yoyote.

Klabu yake ya Yanga leo inashuka dimbani kucheza na JKT Tanzania kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa kwenye uwanja wa Uhuru Dar es salaam saa 10:00 jioni.