Alhamisi , 24th Dec , 2020

Watani wa jadi wa jiji la Manchester Nchini Uingereza vilabu vya Manchester United na Manchester City, vinataraji kuchuana kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Carabao wakati Tottenham Hotspurs imepangwa kucheza na Brentford kutoka ligi daraja la kwanza.

Kushoto ni kocha wa Man United Ole Gunnar Solskjaer na kulia ni Pep Guadiola kocha wa Man City.

Man United imetinga hatua hiyo baada ya kuwaondoa Everton kwa kuwafunga mabao 2-0 kwenye mchezo uliochezwa usiku wa Disemba 23, 2020, na mabao yake kufungwa na washambuliaji Edinson Cavani na Anthony Martial ambaye amefunga baada ya kutokea benchi.

Man City wametinga hatua hiyo baada ya kuwatupa nje Washika mitutu wa jiji la London klabu ya Arsenal kwa kuwafunga mabao 4-1. Pep Guadiola kocha wa Man City anautazama mchezo huo kama nafasi ya kufuta uteja mbele ya Ole Gunnar Solskjaer wa Man United.

Rekodi zinaonesha kocha wa Man United Ole Gunnar Solskjaer anaongoza kumfunga Pep baada ya wawili hao kukutana kwenye michezo 6 kwenye michuano yote  na Solskjaer kuonekana na mbinu bora kwa kumfunga Pep mara 3, sare 2 na Pep akipata ushindi mara 2.

Edinson Cavani wa Man United

Mashetani wekundu klabu ya Man Utd imeweka rekodi ya kuwa timu ya pili kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mara nyingi (16) mara moja nyuma ya Liverpool na ikikumbukwa kutwaa taji hilo kwa mara ya mwisho mwaka 2017 chini ya Jose Mourinho.

Man City ambayo ndiyo bingwa mtetezi imetinga hatua hiyo mara tatu mfululizo na endapo ikifanikiwa kutwaa taji hilo basi itaweka rekodi ya kutwaa taji hilo mara ya 4 mfululizo na Man City kutwaa mara 6 katika miaka 8 ya mwisho.

Gabriel Jesus wa Man City

Michezo ya Nusu fainali ya kombe la Carabao inatazamiwa kuchezwa kuanzia tarehe 4 Januari mwaka ujao kwa mfumo wa mchezo mmoja wa mtoano na sio miwili kama hapo awali na fainali kutazamiwa kupigwa tarehe 25 Mwezi Apil 2021.

Spurs kukipiga na Brentford Nusu fainali kombe la Carabao

Vijana wa Jose Mourinho Masharobaro wa jiji la London klabu ya Tottenham Hotspurs wamepangwa kucheza dhidi ya Brentford baada ya kuwaondoa Stoke City kwa kuwafunga mabao 3-1 usiku wa jana, Harry Kane, Gareth Bale na Ben Davies wakiifungia Spurs.

Spurs wametinga hatua hiyo kwa mara ya pili katika misimu 3 iliyopita na kufukuzia rekodi ya kutaka kutwaa kombe lao la kwanza ikiwa ni baada ya miaka 12 kupita walipofanikiwa kubeba kombe la FA kwa kuifunga Chelsea wakiwa chini ya kocha Harry Redknapp.

Gareth Bale na Harry Kane wa Tottenham

Jose Mourinho ameendelea kuwa na rekodi bora kwenye michuano hiyo baada ya kufuzu kwa mara ya 5 na kufanikiwa kutwaa kombe hilo mara zote 4 ambazo amefanikiwa kuvuka nusu fainali na kucheza hatua ya mwisho ya mtoano ya fainali.

Kwa pande wa Brentford, Brentford kutoka ligi daraja la kwanza wameandika historia ya kutinga nusu fainali yao ya kwanza kwenye michuano hiyo baada ya kuwaondoa Newcastle United kwa kuwafunga bao 1-0 usiku wa juzi na kuwashikisha adabu Westbrom, Soton na Fulham wa ligi kuu.

Michezo ya Nusu fainali ya kombe la Carabao inatazamiwa kuchezwa kuanzia tarehe 4 Januari mwaka ujao kwa mfumo wa mchezo mmoja wa mtoano na sio miwili kama hapo awali na fainali kutazamiwa kupigwa tarehe 25 Mwezi Apil 2021.