Jumatano , 25th Jul , 2018

Michuano ya Sprite Bball Kings mwaka 2018 imefika hatua ya nusu fainali ambapo timu zimeendelea kujiwekea rekodi mbalimbali. Hizi ndio timu 4 zilizotinga nusu fainali ambazo pia ndio zimefunga pointi nyingi zaidi zikiongozwa na Portland.

Timu ya Portland

Portland ambao nusu fainali watacheza na mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars wamejikusanyia pointi 257 kwenye mechi zao tatu za hatua ya mchujo, 16 bora na robo fainali. Walianza kwa kuifunga Eagle Wings pointi 48 kwa 18, kisha wakaifunga KKKT Mbezi Beach pointi 126 kwa 54 na robo fainali wakaifunga Temeke Heroes pointi 83 kwa 70.

Timu ya pili ni Flying Dribblers ambao watacheza na Team Kiza kwenye nusu fainali, wao walianza kwa kushinda pointi 37 kwa 9 za Kurasini Worriors kwenye mchujo, kisha kushinda 87 kwa 63 dhidi ya Ukonga Worriors kabla ya kushinda robo fainali yao kwa pointi 100 dhidi ya 64 za Water Institute.

Mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars, licha ya kucheza mechi mbili tu ambapo walianzia hatua ya 16 bora, wamejikusanyia pointi 201. Walishinda 117 dhidi ya 56 za Osterbay na robo fainali wakashinda kwa pointi 84 dhidi ya 67 za St. Joseph.

Team Kiza ambayo ndio timu ya 4 kwenye nusu fainali yenyewe imejikusanyia pointi 197, katika mechi zake tatu za mchujo, 16 bora na robo fainali. Ilianza kwa ushindi wa pointi 49 dhidi ya 4 za K-Worriors na baadae kushinda pointi 66 kwa 56 za Ukonga Worriors na robo fainali kushinda kwa pointi 82 dhidi ya 47 za DMI.

Mechi za nusu fainali zitapigwa Julai 29, 2018 kwenye uwanja wa taifa wa ndani ambapo mechi ya kwanza itakuwa kati ya Flying Dribblers dhidi ya Team Kiza huku mechi ya pili ikiwa ni kati ya Portland dhidi ya Mchenga Bball Kings.