Jumanne , 14th Jun , 2022

Klabu Yanga itashuka dimbani siku ya Jumatano ya June 15, 2022 kuwakabili Coastal Union ya Jijini Tanga kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia majira ya saa 20:30 usiku.

(Kutoka kushoto, Bakari Mwamnyeto, Djigui Diarra na Kibwana Shomari)

Akizungumza na Wanahabari kuelekea kwenye mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga Mohamed Nasreddine Nabi amethibitisha kuwakosa wachezaji watatu kuelekea mchezo wa kesho kutokana na sababu mbalimbali.

“Tutamkosa Nahodha Mwamnyeto ambaye aliumia kwenye timu ya taifa, Kibwana Shomari ana kadi tatu za njano na Djigui Diarra amefanya mazoezi jana pekee kutokana na kuwa na safari ndefu baada ya majukumu ya timu ya taifa ya Mali lakini wengine watakuwepo” amesema kocha Nabi

Nabi amesisitiza kutambua ugumu wa mchezo wa kesho ambapo Yanga wakipata ushindi kwenye mchezo wa huo watatangazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi kuu Tanzania bara kwa msimu wa 2021/22

“Ni mechi ngumu na kila mara nawakumbusha wachezaji kuhusu mchezo kwa sababu tutakutana na Coastal mara tatu, kuanzia mchezo wa kesho , fainali ya FA pamoja na mchezo wa Ngao ya Jamii kwa hiyo najua ugumu wa mchezo wa kesho” amesema kocha Nabi