Jumamosi , 1st Aug , 2020

Hii leo majira ya saa moja unusu za jioni kwa saa za Afrika Mashariki dunia itaungana kushuhudia fainali ya 139 ya michuano mikongwe ya Kombe la FA katika uwanja  wa Wembley nchini Uingereza.

Kushoto ni Frank Lampard na mwingine ni Mikel Arteta.

Hapa tunaangazia fainali ya miamba miwili ya jiji la London ‘Northwest London Derby’ kati ya washika mitutu wajukuu wa babu wa kifaransa Arsene Wenger timu ya soka ya Arsenal “the gunners” watakapoumana na mashetani wa bluu timu ya bwenyenye kutoka taifa lenye nguvu la kikomunisti Urusi, Roman Abramovich mmiliki halali wa klabu ya Chelsea ‘the blues’.

Arsenal inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kucheza fainali nyingi za michuano hii, fainali 21 na kubeba taji hili mara 13 zaidi ya timu yoyote nchini humo. Itakumbukwa kuwa mwaka 1980 ndio mara ya mwisho kwa washika mtutu hao wa jiji la London kupoteza  mchezo wa fainali ya kombe la FA kwa bao 1-0 dhidi ya wagonga nyundo wa jiji la London West Ham United. Njia pekee iliyosalia kwa vijana hao wa Mikel Arteta kushiriki michuano ya Ulaya ni kuishinda Chelsea kwenye mchezo wa leo.

Itakumbukwa msimu huu umetamatishwa kwa Arsenal kumaliza nyuma ya timu sita bora ndani ya Ligi Kuu ya nchini Uingereza EPL ikiwa ni mara ya kwanza kwa miaka 25 ya hivi karibuni. Huku takwimu zikieleza kuwa kwa michezo 31 ya hivi karibuni ya kombe la FA, Arsenal imeshindwa kufunga goli ndani mchezo mmoja pekee.

Wakati Chelsea chini ya nahodha wa zamani wa klabu hiyo Meneja Frank Lampard inaenda kucheza fainali ya 14 ya michuano hiyo huku ikiwa nyuma ya Arsenal yenye fainali 21 na Manchester United ikiwa na fainali 20. Chelsea imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya michezo 15 ya hivi karibuni ya michuano hiyo.

Mbali na kutumikia rungu la kutosajili msimu uliopita na kushuhudia vijana kina Tammy Abraham wakiibuka klabuni humo, Chelsea kwa upande wao wameshafuzu tiketi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya UCL kwa kumaliza katika nafasi ya nne katika Ligi Kuu nchini Uingereza EPL.

Je, bahati inaangukia kwa nani leo mjukuu wa Mfalme wa Uhispania Mikel Arteta ama mjukuu wa Malkia wa Uingereza Frank Lampard?