Jumatano , 6th Jul , 2016

Kikosi cha timu ya taifa ya Wales kilicho katika ubora wa hali ya juu kinaivaa Ureno katika mchezo muhimu sana wa nusu fainali ya michuano ya mataifa ya Ulaya kikitaka kuweka historia mpya katika michuano hiyo mikubwa kwa kutinga fainali hii leo.

Wachezaji wa wales wakivaana na wa Ubelgiji .

Wales wanajiandaa kwa mchezo huo mkubwa kabisa katika historia ya nchi hiyo wakati wakiivaa timu isiyotabirika ya Ureno katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa usiku wa leo mjini Lyon ili kusaka nafasi ya kucheza fainali ya michuano ya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa.

Kikosi hicho cha kocha Chris Coleman tayari kinafurahia mafanikio makubwa ya kwanza ya kukumbukwa wakifanikiwa kutinga hatua hiyo ya nusu fainali katika michuano mikubwa tangu walipofanya hivyo mnamo mwaka 1958.

[Uingereza] England ndiyo ilikuwa timu ya mwisho kutoka umoja wa nchi za Umoja wa Falme [UK] kufika hatua ya fainali ya michuano ya kombe la dunia na ubingwa wa Ulaya miaka 50 iliyopita.

Kocha Coleman amesema "tutachukuliwa kama wasindikizaji ama wasiopewa nafasi [underdogs], lakini tunajiamini kwa kila mtu".

Mwenyekiti wa chama cha soka cha Wales Jonathan Ford, amesema wanaamini ndoto yao itatimia na wataandika historia.

Nusu ya wananchi wa zaidi ya milioni 3 wa nchi ya Wales wanaamini kuwa wataifunga Ureno mara baada yakuitoa timu ngumu ya Ubelgiji kwa mabao 3-1 katika mchezo wa robo fainali.

Mfalme wa nchi hiyo ya Wales amewatumia ujumbe mzito wachezaji wa timu hiyo akiwatakia kheri ya kushinda mchezo huo na amesema watu wote wako nyuma ya timu hiyo.