Waziri Mwakyembe aleta mjadala utakaobana vigogo 

Ijumaa , 14th Feb , 2020

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa kuna haja ya wadau wa soka kwa pamoja kujadili kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni katika ligi pamoja na manufaa yake.

Waziri Mwakyembe na wachezaji wachezaji wa Simba na Yanga

Dkt. Mwakyembe amesema kuwa ameleta mjadala huo kufuatia malalamiko mengi juu ya uwezo wa wachezaji wa kigeni nchini kuwa mdogo ilihali wakiwa ni kwa idai ya wachezaji 10 na kupelekea kudidimiza vipaji vya wachezaji wa ndani.

"Soka la ushindani nchini ni kwa Simba na Yanga lakini sio sawa kuona wachezaji wa ndani wanalipwa laki 4 halafu wa nje wanalipwa milioni 12 au 13 wakati ukiona mchezo uwanjani, wachezaji wa ndani wanacheza kwa kiwango cha juu na vigogo wanahangaika", amesema Waziri Mwakyembe.

"Tufungue huu mjadala, tuendelee kuzungumza. Mimi naenda mbele ya Bunge kuomba pesa kwa ajili ya kulea vipaji lakini nikiulizwa vipaji ninvyoviombea pesa navipeleka wapi nashindwa kujibu kwasababu huko juu watu wanasajili wachezaji wa nje tena bila kufuata vigezo", ameongeza.

Sheria ya sasa ya usajili wa wachezaji wa Kimataifa inaziruhusu klabu kusajili wachezaji 10 kutoka nje ya Tanzania huku kigezo cha wachezaji wa nje ya Afrika kusajiliwa ni angalau awe anacheza ligi daraja la nne na kuendelea katika nchi husika.