Jumatano , 13th Feb , 2019

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kuwa kitu kikubwa kilichopelekea Manchester United kufungwa katika mchezo wa Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya PSG ni kutokana na kutomiliki mpira.

Kocha Arsene Wenger na wachezaji wa PSG na Man United

Wenger amesema hayo alipokuwa akifanya uchambuzi na kituo cha beIN SPORTS, ambapo amesema timu inapokuwa mwenyeji wa mchezo inahitaji kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa ili iweze kushinda na isipofanya hivyo lazima timu iwe kwenye matatizo.

"Manchester United ilitawala katika idara ya kiungo, lakini PSG ilicheza na viungo watano ambao hawakuwa wakipoteza mpira, Man United haikuwa na uwezo wa kupokonya mipira na pindi inapoupoteza ilikuwa ikipoteza kwa haraka kwasababu PSG ilitawala vizuri katika kurudisha mipira", amesema Wenger.

"Unapocheza nyumbani na huwezi kukaa na mpira, ni lazima utakuwa katika matatizo na hicho ndicho kilichotokea katika mchezo wa leo ( jana ), ambapo Man United imeoneka kuwa na udhaifu katika idara ya kiungo ukilinganisha na PSG ambao walikuwa bora", ameongeza.

Manchester United imepoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora katika uwanja wake wa nyumbani kwa mabao 2-0, ambapo mchezo wa marudio inahitaji kushinda ugenini kwa mabao 3-0 au zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.