Yanga itakavyokamilisha ujenzi, viwanja na M/Makuu

Jumatatu , 23rd Mar , 2020

Klabu ya soka ya Yanga ipo katika mpango mkubwa wa ujenzi wa kituo cha soka pamoja na ofisi za Makao Makuu ya klabu katika vipindi tofauti kuanzia hivi karibuni.

Eneo la viwanja vya Yanga vitakapokamilika

Kituo hicho kitakachojengwa katika eneo lao lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, kitakuwa na jumla ya viwanja viwili vya mazoezi vya soka, hosteli za wachezaji pamoja na bwawa la kuogelea lenye viwango vya Olympic pamoja na viwanja vya Mpira wa Kikapu na Mpira wa Pete.

Akizungumzia kuhusu mipango hiyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ujenzi na Miundombinu wa klabu hiyo, Said Mrisho amesema kuwa kila kitu kipo sawa na kinachosubiriwa ni mvua kupungua ili kuanza kwa awamu ya kwanza ya ujenzi ambayo itahusisha viwanja hivyo viwili.

"Tunataka kuanza kujenga viwanja viwili vitakavyokidhi vigezo vya FIFA na CAF na kuandaa mashindano ya Kimataifa ya U-17 na timu yetu ya wanawake, cha kwanza ni cha nyasi bandia na kingine ni cha nyasi asilia", amesema Mrisho.

"Utekelezaji haufanyiki kwa pamoja, utaenda kwa hatua ambapo kwa mwaka huu sisi kama kamati tumeshauri tuanze na viwanja vya mazoezi na suala la upatikanaji wa fedha ni la uongozi wa klabu. Mungu akipenda mvua zikiisha tutaanza ujenzi na mpaka kufikia Disemba mwaka huu utakuwa umekamilika", ameongeza.

Kuhusu suala la kurekebisha ofisi za Makao Makuu ya klabu hiyo, Said Mrisho amesema kamati yake imeshauri kuwa suala la ujenzi wa ofisi mpya katika eneo la Makao Makuu litafuata baada ya kukamilika kwa mradi wa serikali katika eneo la Jangwani na kwamba hivi sasa nguvu kubwa inaelekezwa Kigamboni.