Yanga, Simba na Azam FC zote zimemuita Masau Bwire

Jumatano , 11th Dec , 2019

Msemaji wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting Masau Bwire ambaye ameweka wazi kuwa kwasasa yeye ni mkurugenzi wa klabu hiyo, amesema ameshawahi kuhitajiwa na klabu kongwe za Yanga na Simba.

Msemaji wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting Masau Bwire

Bwire ameyasema hayo leo kwenye Kipenga Xtra ya East Africa Radio lakini amesema hakuwahi kukubali kwasababu ana heshimu nafasi yake ndani ya Ruvu Shooting.

'Klabu za Yanga, Simba na Azam FC zimeshanifuata mara kadhaa kutaka nikawe msemaji wao, lakini kwa yale ambayo Ruvu Shooting imeshanifanyia tangu mwaka 2001 na hivi sasa mimi ni Mkurugenzi sioni namna ya kuachana nayo' - Masau Bwire.

Kwa upande mwingine Masau Bwire ameeleza kuwa Ruvu Shooting kwasasa ni kampuni na ina wana hisa pamoja na wakurugenzi 8 akiwemo yeye.

'Sisi Ruvu Shooting ni kampuni kwasasa na tuna usajili kamili wa Brela, hivyo tunashirikiana na watu ambao wananunua hisa na kufanya klabu ijiendeshe kwahiyo kwasasa sio timu ya jeshi moja kwa moja' - Masau Bwire

'Mimi ni miongoni mwa wakurugenzi wanane wanaoiongoza klabu ya Ruvu Shooting ila nimepewa hiki kitengo cha habari kwasababu mdomo wangu ni mwepesi kidogo kuongea'- Masau Bwire.