Yanga yatangaza kocha mpya, fahamu historia yake

Alhamisi , 9th Jan , 2020

Mabingwa wa kihistoria Yanga SC wamemtangaza kocha Luc Eymael raia wa Ubelgiji kuwa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo baada ya kuachana na kocha Mwinyi Zahera.

Luc Eymael

Kocha huyo anakuja kuifundisha Yanga akitokea klabu ya Black Leopards ya nchini Afrika Kusini.

Historia yake kwa ufupi.

Luc Eymael alizaliwa Septemba 20 mwaka 1959 nchini Ubelgiji, ambapo alianza kucheza soka mwaka 1975 katika klabu ya Royal Star Fléron FC ya ligi daraja la nne nchini Ubelgiji.

Alianza kazi ya kufundisha soka mwaka 1999 katika klabu ya  Lierneux ya ligi daraja la tano nchini Ubelgiji, alipata leseni ya ukufunzi ya UEFA Pro mwaka 2007. Klabu alizofundisha barani Afrika ni pamoja na AS Vita ya DR Congo, Missile ya Gabon, MC Oran ya Algeria, AFC Leopards (Kenya), Rayon Sports (Rwanda), Al-Merrikh (Sudan), Polokwane City na Free State Stars za Afrika Kusini.

Amefanikiwa kushinda ubingwa wa ligi katika klabu za AS Vita, Missile, AFC Leopards, Rayon Sports na mafanikio aliyonayo katika michuano ya vilabu barani Afrika ni kufika hatua ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.