Jumatano , 21st Feb , 2018

Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara klabu ya Yanga leo imefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya St. Louis ya Shelisheli kwenye mchezo uliomalizika jioni hii.

Yanga imeiondoa St. Louis kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kushinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam wiki iliyopita. Bao la Yanga leo limefungwa na kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib Migomba dakika ya 45 akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Hassan Kessy.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa kutoka  Madagascar, Andofetra Avombitana Rakotojaona aliyesaidiwa na Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy, hadi maopumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, Yanga itakutana na mshindi kati ya El Merreikh ya Sudan au Township Rollers ya Botswana. Kwenye mchezo wa kwanza Township Rollers ilishinda mabao 3-0 nyumbani.

Timu nyingine ya Tanzania inayoshiriki michuano ya Kombe la shirikisho Afrika Simba imesonga mbele baada ya kushinda kwa mabao 5-0 dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti.