Jumatano , 12th Mei , 2021

Kikosi cha mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara Yanga SC, kimefika salama Mkoani Mtwara leo Asubuhi, ikiwa ni maandalizi kueleka mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Namungo.

Wachezaji wa Yanga Saidi Ntibazonkiza kulia na Fiston Abdul Razak kushoto wakiwa uwanja wa ndege wa Mtwara

Mchezo huu utachezwa siku ya Jumamosi Mei 15, 2021 katika dimba la Majaliwa huko Ruangwa mkoani Lindi. Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara ikiwa na alama 57 ikiwa ni tofauti ya alama 4 dhidi ya Simba amabao ndio vinara wa VPL, wakati Namungo wapo nafasi ya 11 wakiwa na alama 32.

Yanga itashuka dimbani kwa mara ya kwanza tangu Aprili 30 ambapo ilicheza mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Tanzania Prisons mchezo ambao walishinda kwa bao 1-0. lakini baada ya hapa walipaswa kucheza dhidi ya watani zao Simba Mei 8 mchezo ambao ulihairishwa kutokana na mkanganyiko wa ratiba na sasa utapangiwa tarehe mpya.

Namungo kwa upande wao kabla ya mchezo dhidi ya Yanga siku ya Jumamosi, leo wanakibarua Saa 10:00 jioni katika dimba la Majaliwa dhidi ya Mtibwa Sugar.

Na kwenye rekodi kuelekea mchezo wa Namungo dhidi ya Yanga zinaonyesha, kwenye michezo mitatu ya ligi waliokutana hakuna timu iliyoshinda mchezo hata mmoja michezo yote ilimalizika kwa sare ikiwemo mchezo wa mkondo wa kwanza msimu huu ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 1-1.