Alhamisi , 17th Jan , 2019

Kocha wa Yanga raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera, amesema kutokana na uzoefu wa klabu ya AS Vita anaamini Simba itapata wakati mgumu japokuwa ina wachezaji wazuri.

Mwinyi Zahera, Chama na Patrick Aussems

Akifanya mahojiano na www.eatv.tv Zahera amesema wachezaji wa AS VIta Club wengi wana uzoefu wa kucheza mashindano makubwa na kukutana na timu kubwa hususani wale wanaocheza timu ya Taifa ya DR Congo ambayo yeye ni kocha msaidizi.

''Kuna wachezaji 6 wa Vita Club wanacheza timu ya taifa ya DR Congo na wamezoea kucheza mechi na mataifa makubwa kama Ivory Coast na Morocco hivyo wanakutana na wachezaji wakubwa hawawezi kumwogopa Chama'', amesema.

Zahera pia ameeleza kuwa timu zote, Simba na Vita Club zinawachezaji wazuri tofauti ni kwamba uendeshaji wa Vita Club ni kama Ulaya na wamepiga hatua kubwa na tayari walikuwa na watu wa kuifutilia Simba kuanzia ikiwa Zanzibar kwenye Mapinduzi Cup mpaka ilipokuja kucheza na JS Sauora.

Simba imeondoka nchini leo kuelekea nchini DR Congo kwaajili ya mchezo huo wa pili kundi D utakaopigwa Jumamosi saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.