Kampeni hii kubwa na ya aina yake ina malengo mazuri kwa mustakabali wa Taifa, ni kuwakumbusha na kuwaelimisha vijana kuhusiana na umuhimu pamoja na uwezo walionao katika kufanya maamuzi sahihi kwenye masuala makubwa ya kitaifa hususani yanayohusu siasa za nchi yetu Tanzania.
Dhamira ya kampeni hii, ni kuwahimiza vijana kutumia fursa waliyonayo katika kufanya maamuzi katika mambo makuu mawili.
Kwanza, kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili ifikapo Oktoba, kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura ili kuchagua viongozi wao ambao ni madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nchini mwetu, umri rasmi wa mpiga kura ni kuanzia miaka 18 na kuendelea, na kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, jumla ya watu 22,424,136 wana umri wa kushiriki zoezi hilo kwa mwaka huu.
Katika idadi hiyo ya wapiga kura, vijana wenye umri wa miaka 18 mpaka 40 peke yao ni 15,293,681, idadi ambayo ni sawa na asiilimia 68.20 ya wapiga kura wote.
Hii ina maanisha kwamba hatma, ama mustakabali wa Taifa hili uko mikononi mwa vijana. Na ndio maana kituo cha EATV na East Africa Radio ambavyo vinaaminika zaidi na vijana, vimeamua kuchukua jukumu la kuendesha kampeni hii kwa kutambua umuhimu na nguvu ya vijana katika Taifa letu
Na ili kuendeleza zoezi la kuwahamasisha vijana, leo tukiwa pamoja na kundi la Weusi na mtayarishaji Nahreel tunazindua wimbo ya Zamu Yako. Tunaimani wimbo huu utazidi kuimarisha kampeni ya ‘Zamu Yako’ na kuweza kufanikisha dhamira zake.