
Kiungo Jonas Mkude ambaye ni mara yake ya kwanza kuitwa katika kikosi hicho chini ya kocha Boniface Mkwasa amesema, ni kipindi kigumu kwasababu Algeria ni timu kubwa ambayo ipo katika ubora wa juu Afrika lakini wanaamini watafanya vizuri kwa juhudi zake na juhudi za timu nzima pamoja na kocha kama wakiweka dhamira ya kitu wanachokifanya.
Mkude amesema, katika timu ushindani ni muhimu na ataweka bidii katika mazoezi ila kocha ndiye muamuzi wa mwisho na hata akipata au akikosa namba katika kikosi wanachoamini ni ushindi kwa ajili ya kuiwakilisha nchi.
Kwa upande wake mshambuliaji Ramadhan Kessy amesema, kuitwa kwenye timu ya taifa ni changamoto kubwa kwani kunaupinzani mkubwa lakini kinachotakiwa ni kufuata maelekezo yote anayotoa kocha kwa ajili ya timu na sapoti kwa wachezaji ndiyo itakayowawezesha kufanya vizuri katika michezo iliyo mbele yao.
Stars imeondoka ikiwa na kikosi cha wachezaji 24, pamoja na bechi la ufundi linalongozwa na kocha mkuu Charles Boniface Mkwasa.
Wachezaji waliondoka ni Ally Mustafa, Aishi Manula, Said Mohamed, Juma Abdul, Shomari Kapombe, Ramadhan Kessy, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Salim Mbonde, Kelvin Yondani na Nadir Haroub.
Wengine ni Mudathir Yahya, Frank Domayo, Himid Mao, Salum Abubakar, Farid Mussa, Saimon Msuva, Salum Telela, Jonas Mkude, Said Ndemla, Ibrahim Hajibu, Malimi Busungu na John Bocco.
Mshambuliaji wa Stand United, Elias Maguri anatarajiwa kuungana na kikosi hicho kesho baada ya kuitumikia timu yake katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara leo jumatatu dhidi ya Mgambo Shooting katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Kwa upande wa washambuliaji Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa wanaocheza soka nje ya nchi, wataungana na wenzao baada ya michezo ya mwishoni mwa wikiendi hii.