
Hayo yamesemwa Mkoani Dodoma na Mh. Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii,Jinsi,Wazee na Watoto kwenye uzinduzi wa kituo cha matibabu kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuongeza kuwa ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya Halmashauri hasa zile mpya hawana hospitali, hali inayosababisha wagonjwa wengi kutibiwa katika Hospitali za Rufaa ngazi ya Mkoa na hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa katika Hospitali hizo.
Amesema kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ya "HAPA KAZI TU" ni kuboresha huduma kwa kuzingatia uwazi, uadilifu na uwajibikaji wenye matokeo makubwa.
Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI itaendelea kuimarisha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya ili kuleta uwiano wenye kuleta tija ya upatikanaji wa huduma bora.
Ametaka Jamii na Wananchi kwa ujumla kuilinda miundombinu ya vituo mbalimbali vya afya visiharibiwe na jukumu hilo amehimiza kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili vituo mbalimbali nchini vinavyojengwa kwa lengo la kuhudumia jamii vitunzwe na kudumu.
Waziri Ummy amesema mbali na usafi ni vyema suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wake lizingatiwe na kupewa umuhimu mkubwa ni vema kituo hicho kianze na ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki ili kuboresha makusanyo na kuzuia mianya ya kuvujisha mapato hayo.
Aidha, ameagiza kwamba fedha zinazotokana na Mifuko ya Maendeleo ya Jamii zitumike kuboresha huduma katika vituo mbalimbali na hasa ununuzi wa dawa za ziada kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na asilimia 50 ya fedha hizi zitumike kununua dawa ili kuhakikisha dawa muhimu zote zinapatikana kutoka Bohari Kuu ya Dawa kwa bei nafuu na kwa wakati.
"Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa watanzania wote kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji wenye matokeo mazuri. Uboreshaji huu ni katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo uwepo wa wataalamu wa kutosha na wenye kuzingatia miiko na maadili ya taaluma zao, vifaa tiba, miundombinu na upatikanaji wa huduma za dawa," alisema Mhe. Ummy.