Mshambuliaji wa Stand United, Elias Maguli
Mwadui ambayo ipo chini ya kocha Jamhuri Kihwelo Julio inajaribu kuimarisha kikosi chake hasa katika nafasi ya ushambuliaji hasa kutokana na kufunga magoli 29 katika msimu huu ikiwa imecheza mechi zote 30.
Maguli amekuwa hana nafasi nzuri katika kikosi cha Stand mara baada ya kuingia kwenye mgogoro na kocha wake Patrick Liewig baada ya kwenda kufanya majaribio nchini Misri huku kocha wake akiwa hana taarifa hizo.
Baada ya Maguli kurejea Stand, hakupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza licha ya kuwa ndiye mshambuliaji aliyekuwa akiongoza kwa kuzifumania nyavu katika ligi kwa wakati huo hadi baadaye alipoomba radhi.
Endapo Maguli ataihama Stand United, inatajwa kuwa maelewano madogo kati yake na Liewig ndiyo sababu kubwa ya nyota huyo wa taifa stars kuikacha Stand ambayo ameifungia magoli 14 katika msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo akishikilia nafasi ya nne katika orodha ya wafungaji bora wa VPL msimu uliomalizika hivi karibuni.
Idd Ubwa na Haruna Chanongo ni wachezaji wengine ambao waliingia kwenye marumbano na kocha huyo mfaransa.
Maguli alishawahi kuvitumikia vilabu vya Tanzania Prisons, Ruvu Shooting na Simba.
