Jumanne , 1st Nov , 2016

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe.Mhandisi Gerson Lwenge amezitaka wilaya zote nchini kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua ili kukidhi mahitaji ya maji hasa nyakati za ukame na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yao.

Mhandisi Gerson Lwenge - Waziri wa Maji na Umwagiliaji

 

Akiongea na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wadhibiti wa Huduma za Maji Kusini na Mashariki mwa Afrika (ESAWAS), Mhe. Gerson Lwenge amesema mabwawa hayo yatasaidia kupatikana maji hasa vipindi vya ukame na maeneo ya vijijini ambako hakuna miundombinu ya maji safi na salama.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Mbogo Futakamba amebainisha kuwa serikali ya awamu ya tano imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya maji ambapo mpaka sasa imeshakamilisha ujenzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini unaosambaza zaidi ya lita za maji  milioni 200 kwenye mkoa wa Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi amesema kuwa kuwepo kwa vyombo vya udhibiti wa huduma za maji kama vile ESAWAS vitasaidia kuondoa migogoro kati ya watumia maji na watoa huduma za maji.