Jumapili , 5th Feb , 2017

Azam FC, inashuka dimbani leo kuvaana  na Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumapili saa 1.00 usiku.

Ndanda walipokutana na Azam msimu uliopita

Kuelekea mchezo huo, wachezaji wa Azam FC wamejipanga vilivyo kufanya kweli kwa kuibuka na ushindi kufuatia mafunzo makali wanayopewa na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, Msaidizi wake Idd Cheche na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar.

Ndanda FC nao wanataka kuendeleza ubabe wa kuichapa Azam, baada ya ushindi wa 2-1 iliyoupata katika mchezo wake wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Nngwanda Sijaona Mjini Mtwara.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Azam zinasema kuwa kikosi chao kipo fiti lakini kitakuwa na pengo la wachezaji wake wanne waliokuwa wagonjwa ambao ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, viungo Stephan Kingue, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na beki wa kulia Shomari Kapombe.

Hadi timu hizo zinakutana, Azam FC ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 34, ikiwa nyuma ya pointi 15 na kinara Yanga aliyejikusanyia 49, Ndanda yenyewe ipo kwenye hatari ya kushuka daraja baada ya kujizolea pointi 19 ikiwa nafasi ya 15.

Kihistoria kwenye mechi za ligi timu hizo zimekuwa na upinzani mkali, ambapo Azam FC imekutana na Ndanda mara tano na kushinda mechi mbili sawa na timu hiyo huku ikishuhudiwa mchezo mmoja ukiisha kwa sare.