Jumatano , 21st Feb , 2018

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutoa kauli juu ya watu 40 waliokamatwa kwenye maandamano ya chama hicho Februari 16, 2018 katika eneo la Magomeni Jijini Dar es Salaam.

Mnyika ameeleza hayo jioni ya leo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupita takribani siku tano tokea kwa watu hao kukamatwa na kuweka ndani ambapo amedai endapo Polisi wakishindwa kuwapa dhaman na kuwatolea ufafanuzi hadi ifikapo kesho basi wapelekwe Mahakamani.

"Jeshi la Polisi mpaka hivi sasa wamekwisha vunja sheria kwa kutowapa dhamana wala kuwafikisha Mahakamani. Tunalitaka Jeshi la Polisi kupitia kwa IGP na Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, kutoa kauli leo juu ya hao ambao wanawashikilia na kuwanyima dhamana na kutowafikisha Mahakamani", amesema Mnyika.

Pamoja na hayo, Mnyika ameendelea kwa kusema "Jeshi la Polisi litoe tamko kwa kuidhinisha kwa majina watu wote 40 na kama kuna wengine vile vile wanawashikilia wawataje kwa majina na waeleze taratibu za kuwapa dhamana ya kipolisi na kama hawawezi hilo basi kesho asubuhi wawapeleke Mahakamani ili waweze kupewa haki yao".

Kwa upande mwingine, Mnyika amedai kwa mujibu wa taarifa walizokuwa nazo Jeshi la Polisi liliwakamata watu wengine ambao walikuwa wanajishughulisha na shughuli zao huku wengine wakiwa wametoka kushuka kwenye madaladala.