Alhamisi , 16th Aug , 2018

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, likiongozwa na Kamanda, Ulrich Matei  linawasaka watu wanaodaiwa kufanya uharibifu wa miundombinu ya maji katika Kijiji cha Ngole, Kata ya Ilungu wilayani Mbeya.

Kamanda wa Polisi jijini Mbeya, Ulrich Matei.

Hatua inakuja ikiwa ni siku moja imepita baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila,  kutoa agizo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Paul Ntinika, kuwa wakamatwe wanakijiji wote kutokana na uharibifu wa miundombinu ya mradi wa maji.

Inadaiwa kuwa uharibifu uliofanywa  katika Kijiji cha Mashesye ni kukata mabomba yaliyokuwa yametandazwa kuanzia kwenye chanzo cha maji.

Kutokana na agizo hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali huko katika kijiji cha Ngole kuhakikisha wale wote waliohusika na uharibifu huo wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi.

Mwenyekiti wa Kijiji  cha Mashesye ambacho kiliharibiwa miundombinu ya maji,  Lazaro Mwakalila, amedai kuwa wananchi  wa  Kijiji cha Ngole wakiwa na Mwenyekiti wao walifika eneo lake na kukata mabomba ya maji na kubomoa tanki la maji wakitumia vifaa mbalimbali yakiwamo majembe na mapanga.

Agizo hilo linakuja ikiwa ni siku chache tangu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo kukemea tabia ya baadhi ya Wakuu wa Wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo kuwaweka watu ndani.

Jafo alisema hayo jijini Dodoma kwenye kikao kazi na wakuu wa Wilaya 27 walioteuliwa hivi karibuni kilicholenga kuwapa maelekezo ya kazi, ambapo Jafo alisema, tabia hiyo inasababisha wananchi kuichukia serikali, hivyo ameagiza Wakuu wa Wilaya kutumia sheria hiyo kama ilivyokusudiwa na siyo kwa kuonea watu.

Msikilize hapo chini Kamanda, Ulrich Matei ameeleza zaidi kuhusiana na tukio hilo.