Jumatatu , 26th Nov , 2018

Baada ya hivi karibuni kubainika kuwa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar haijalipwa fedha zake za kushinda ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho, kiasi cha shilingi milioni 50, pande mbili husika ambazo ni TFF na mdhamini, zimeendelea kutupiana mpira.

Mtibwa Sugar walipokabidhiwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

Kwa upande wa TFF wao wameweka wazi kuwa suala hilo la kukabidhi zawadi, lipo kwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo ambao ni kampuni ya Azam.

''Nadhani ni vizuri kuwasiliana na mdhamini hili suala la zawadi lipo chini yake'', alisema Afisa mmoja wa TFF kwenye mahojiano maalum kwa sharti la kutokutajwa jina lake.

Jibu hili la TFF linaibua hofu juu ya kutotoka kwa zawadi hiyo baada ya hivi karibuni upande wa mdhamini nao kuweka wazi kuwa wao wameshatimiza wajibu wao na suala hilo lipo chini ya TFF.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar wao wamekuwa wakikataa kuzungumzia suala hilo pamoja na kukiri kuwa hawajapata fedha hizo, lakini wamekuwa wakisisitiza kuwa ufafanuzi zaidi upo TFF na kwa mdhamini jambo ambalo linazidi kuleta sintofahamu juu ya nani hasa anayestahili kukabidhi zawadi kwa mshindi.