Jumapili , 9th Dec , 2018

Msanii wa filamu nchini, Irene Uwoya ambaye amewahi kuwa mke wa mwanamuziki Dogo Janja, amesema kuwa anachokifanya msanii huyo kwa sasa ni kizuri na kinatakiwa kiendelezwe ikiwa ni katika kurudisha msaada kwa jamii yake.

Msanii wa filamu nchini, Irene Uwoya, akiwa na Dogo Janja.

Uwoya amezungumza hayo katika uzinduzi wa filamu mpya ya msanii mwenzake, Gambo Zigamba ambapo amesema kuwa suala la kutoa misaada kwa jamii ni jambo jema na ambalo linatakiwa kuwekewa muendelezo.

"Ni kitu kizuri kufanya vile maana inarudisha fadhila kwa mashabiki, na anatakiwa kuendeleza zaidi na zaidi", amesema Uwoya.

Mbali na Dogo Janja kumkabidhi mama yake mzazi nyumba aliyomjengea, pia alirudi kwenye shule ya msingi aliyosoma jijini Arusha, shule ya msingi Ungalimited na kutoa ndoo ishirini za rangi pamoja na kukarabati shule hiyo kwa kuezeka mabati.

Ikumbukwe kuwa wawili hao walikuwa kwenye mahusiano ambayo yalipelekea hadi kufunga ndoa, lakini siku za karibuni ukaribu wao umepungua ambapo inasemekana kuwa wameachana kutokana na kila mmoja kufanya mambo yake mwenyewe.

Hakuna kati yao aliyethibitisha kuachana kwao lakini Irene Uwoya hivi karibuni aliwahi kusema kuwa hakuwahi kubadili dini na kuwa Muislamu, hali inayoonesha kuwa mapenzi yao sasa yamefikia mwisho.