Jumatatu , 11th Nov , 2019

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema chama hicho kwa sasa kinaendelea kufuatilia muenendo wa zoezi zima la uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kinatarajia kutoa tamko lake Novemba 13, 2019.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Polepole ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter, ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, kutoa tamko la kuwarejesha wagombea wa upinzani, ambao vyama vyao vilitangaza kujiondoa na pamoja na kueleza CCM kupita bila kupingwa kwenye Vijiji vingi.

"Tunaendelea kufuatilia maendeleo ya mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Chama Cha Mapinduzi kitatoa kauli siku ya Jumatano Tarehe 13 Novemba 2019." ameandika Polepole.

Mapema jana akizungumza na waandishi wa habari Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, alisema mchakato mzima wa zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaendelea kama kawaida kwa kuwa wadau wote walishashirikishwa awali na kupewa kanuni.

"Wagombea ambao waliteuliwa na vyama vyao wakafanikiwa kuchukua na kurejesha fomu, kwa kipindi kilichopangwa na wamerejesha watu hao wana haki ya kugombea, hakuna kuweka mpira kwapani." alisema Jafo.