Jumatatu , 16th Dec , 2019

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Wallace Karia amewataka mashabiki wa soka nchini kuipa sapoti timu yao ya taifa 'Kilimanjaro Stars' iliyopo nchini Uganda kwenye michuano ya CECAFA.

Rais wa TFF, Wallace Karia na baadhi ya wachezaji wa Kilimanjaro Stars

Michuano hiyo hivi sasa ipo katika hatua ya nusu fainali ambapo Kilimanjaro Stars itashuka dimbani kesho Jumanne dhidi ya wenyeji Uganda.

Rais wa TFF amesema, "niwaambie Watanzania timu zetu zilipofikia zinastahili pongezi kwa kazi kubwa waliyoifanya, tuwape moyo na tuwaombee dua angalau tuweze kufanya vizuri zaidi ya hapa. Nia yetu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa washindani kwenye kila mashindano tunayoshiriki".

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda amesema kuwa kucheza kwa kutafuta pointi ni tofauti na kucheza kwenye mtoano, hivyo watafanyia kazi mapungufu ya kikosi cha Uganda ili waweze kufanya vizuri.

Pia amesema kikosi chake kinakabiliwa na majeraha ya mshambuliaji Miraji Athumani ambaye ameumia kifundo cha mguu katika mchezo uliopita lakini anaendelea vizuri na hivi sasa amepumzishwa.

Kilimanjaro Stars ni mabingwa mara tano wa michuano hiyo na endapo watafanikiwa kuchukua ubingwa nchini Uganda mwaka huu itakuwa ni mara ya sita, ambapo mwaka 2010 ndiyo mara ya mwisho kwa Stars kushinda ubingwa huo unaozikutanisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.