
Wanyama katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi hiyo Pascal Shelutete, imesema hii ni mara ya pili kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushinda katika kundi la hifadhi zinazoongoza kwa ubora bara la Afrika baada ya kushinda mwaka 2019.
Tuzo hizo zimezotolewa na Taasisi ya World Travel Award, (WTA) ya nchini Marekani ambapo Hifadhi ya Serengeti ilizishinda hifadhi nyingine kwenye kinyang'anyiro hicho ambazo ni Centeral Kalahari, (Botswana),Etosha (Namibia), Kidepo Valley (Uganda),Kruger (Afrika Kusini)na Maasai Mara National Reserve (Kenya).
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),limeishukuru serikali ya Tanzania pamoja na wadau wa Utalii pamoja na wananchi wote waliopiga kura na kuifanya Serengeti kuwa Hifadhi bora zaidi barani Afrika kwa mwaka 2020.
Serengeti inajivunia umaarufu wa msafara wa nyumbu wahamao zaidi ya milioni moja na nusu, aina mbalimbali za wanyamapori wanaopatikana kwa wingi, mandhari nzuri ya kuvutia pamoja na shughuli mbalimbali za utalii zinazovutia watalii wengi.