Alhamisi , 28th Jan , 2021

Timu ya  Taifa  ya Tanzania 'Taifa  Stars' kwa wachezaji wa ndani, imetolewa  katika mashindano ya CHAN yanayoendelea nchini Cameroon, baada ya kupata sare ya 2-2 katika mchezo wa mwisho wa kundi D, dhidi ya  Guinea.

Kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars Etienne Ndayiragije

Taifa Stars ilihitaji ushindi ili iweze kusonga mbele katika  hatua ya robo fainali. Guinea  ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 4 tu ya mchezo, lakini Taifa Stars walisawazisha dakika ya  29 kwa shuti la mbali nje ya box lililopigwa na Baraka  Majogoro.

Stars ilichangamka zaidi katika kipindi cha  pili  na kufanikiwa kupata bao kunako dakika ya 69, lililofungwa na beki wa kushoto Edward Manyama, kufuatia kona  iliyopigwa na Farid Mussa.

Kama ilivyo mwenye 'bahati habahatishi' Guinea walisawazisha goli kunako dakika 82 kwa bao lililofungwa na Victor Kantabadouna, ambalo lilipelekea ndoto za Stars kusonga mbele kutoweka kabisa, maana Stars alipaswa kupata matokeo ya ushindi tu, sare au matokeo mengine yasinge inufaisha.

Hatua ya robo fainali zinatarajiwa kuanza jumamosi tarehe 30/1/2021 kwa michezo miwili na kumalizika jumapili 31/1/2021 michezo miwili pia.

Ratiba Kamili
30/1/2021     Mali  vs   Congo
 30/1/2021     DR Congo   vs Cameroon
 31/1/2021      Morocco  vs  Zambia
 31/1/2021      Guinea     vs  Rwanda