Ijumaa , 2nd Apr , 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu amesema TAMISEMI si ngumu kama baadhi ya watu wanavyosema isipokuwa ni kubwa lakini utendaji kazi wa pamoja utatoa ugumu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amesema hayo alipowasili  katika ofisi za Wizara hiyo Jijini Dodoma, ambapo amewataka watendaji wa TAMISEMI kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikano, ubunifu, uzalendo na uadilifu ili kurahisisha utendaji kazi.

"Baadhi ya watu wanasema TAMISEMI ni ngumu, mimi nasema sio ngumu, kama TAMISEMI ni ngumu maana yake mmeshindwa kunisaidia mimi na Manaibu Waziri kutekeleza wajibu wetu, ila tunakubali ni kubwa lakini hakuna kigumu kama kuna utendaji kazi wa pamoja,” alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy aliyeapishwa jana kuongoza wizara hiyo amesema atashirikiana na wafanyakazi wa TAMISEMI ili kuonyesha matokeo mazuri katika ukusunyaji wa mapato.

“Sitaki kusema mimi ni hodari bali ni hodari wa kushirikiana na wenzangu naamini tutakwenda vizuri, na kubwa lazima tuonyeshe matokeo hasa kwenye ukusanyaji wa mapato,” alisema Waziri Ummy.