Jumatatu , 3rd Mei , 2021

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amempa onyo mbunge wa Mtama kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kwa kitendo chake cha kuwasema vibaya wabunge wenzake 19 waliofukuzwa uanachama na CHADEMA. 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai

Hayo yamejiri hii leo Mei 3, 2021, Bungeni jijini Dodoma, zikiwa zimepita siku chache baada ya video kusambaa ikimuonesha mbunge Nape akichangia moja ya mjadala uliohusisha wabunge 19 wa Viti Maalumu akiwaita COVID-19 akidai kuwa wamefukuzwa chama na jambo hilo liheshimiwe. 

"Majuzi mdogo wangu Nape yalimtoka maneno kidogo na yamezunguka sana, ikifika mahali mbunge na Spika muanze kupishana naona haipendezi eeh kwahiyo sitopitia hoja zake, kitu kimoja ambacho hana uhuru sababu ya kanuni ni kuwasema vibaya wabunge wenzake, aliwataja kwa majina ya huko mitaani kwakweli alikosea sana", amesema Spika Ndugai

"Niliongea naye naamini aliteleza, ninachowaomba mumsamehe bure mtu akikufanyia kosa kubwa sana unachoweza kufanya ni kumsamehe bure aliwakosea sana, tuchunge sana midomo yetu tunapo-deal na binadamu wenzetu, Nape unapo-deal na wanawake Duniani kote unaongea nao kwa heshima", ameongeza Spika Ndugai