Jumatano , 9th Mar , 2022

Jeshi la Uhamiaji mkoani Iringa kwa kushirikiana na ofisi ya Mamlaka ya Mapato mkoani humo (TRA) limewakamata wahamiaji haramu 78 raia wa Ethiopia na Watanzania wawili.

Baadhi ya wahamiaji haramu waliokamatwa

Akithibitisha kukamatwa kwa wahamiaji hao Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji mkoani Iringa Agnes Luziga, amesema raia hao wamekamatwa jana Machi 8, 2022, majira ya saa 1:00 jioni.

Luziga ameeleza kuwa jana jioni alipata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna gari linasadikiwa kubeba wahamiaji haramu ambalo katika gari hilo kulikuwa na ‘seal’ ya TRA ambayo ilikuwa sio rahisi kwa mtu kugundua.

"Wahamiaji tuliowakamata ni raia wa Ethiopia wametokea Ethiopia kupitia mpaka wa Hororo-Taveta wakielekea nchini Afrika Kusini wakienda kutafuta maisha, hivyo taratibu za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hawa zinaendelea," amesema Agnes.