Alhamisi , 28th Apr , 2022

Watu wanne ambao ni askari wa Jeshi la Polisi wawili na mahabusu wawili wamefariki dunia, kwenye ajali iliyotokea katika kijiji cha Ibanda  mkoani Geita.

Ajali hiyo imetokea April 27 majira ya saa 10:00 jioni   ikihusisha gari la  Polisi namba PT 3798 Toyota Landcruiser lililokuwa likitokea Geita kusikiliza kesi mahakamani,  kugongana na Lori aina ya Scania namba T 691 DBQ mali ya kampuni ya Nyanza lililokuwa likitokea mkoani Mwanza kuelekea mkoani Geita. 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Henry Mwaibambe ameeleza chanzo cha ajali hiyo kuwa ni gari la Polisi kupata hitilafu.

Mganga Mfawidhi hospitali ya rufaa mkoa wa Geita dokta Mfaume Salum anasema alipokea majeruhi watatu na wote wamepatiwa matibabu mmoja anaweza kuruhusiwa.