Jumatano , 15th Jun , 2022

Nkeya Thomas mtoto wa miaka miwili mkazi wa Kijiji cha Nyamigogwa kata ya Shabaka wilayani Nyanghwale mkoani Geita ameuwawa kikatili kwa kukatwa shingo na watu wasiojulikana.

Akizungumza  baada ya mazishi mama wa mtoto huyo Mperwa Sayari ameeleza jinsi alivyoshuhudia mwili wa mwanae ukiwa umekatwa shingo na watu wasiojulikana na  kuubeba kuupeleka nyumbani.

"Niliamka asubuhi nikawakorogea uji wakanywa, baada ya hapo nikaenda kilioni saa 4 asubuhi , ilipofika saa 7 mchana nikarudi nyumbani kwa sababu nina mtoto mchanga, nilipofika nikafua Madaso, nilipofua Madaso, bado nafua kakafika katoto ka shemeji kakanambia  mama kule J amechinjwa, nikauliza wapi nipeleke akakimbia ghafla akanipeleka mpaka alipokuwa mtoto, nikafika kweli nikamuona, mtoto wangu amelala chali, kakatwa shingo"


Nilivyofika nikambeba mabegani nakuja nae nyumbani, nikapiga mwano sasa, majirani badae wakafika wakakuta nimembeba mwanangu mgongoni, wakasema mama  imekuwaje, nimekuta mwanangu amechinjwa, wakambeba wakampeleka ndani", alisema Sayari

Aidha Mkuu wa wilaya ya Nyanghwale Jamhuri William amechukizwa na tukio hilo lililopelekea kukatiza uhai wa mtoto huyo, huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili waweze kumpata mtu aliyefanya tukio hilo.

"Mtu anaechukua uhai wa mtoto kama huyu, ambae ni malaika wa Mungu, ametenda kosa kubwa sana, mimi Mkuu wa wilaya nalaani kwa nguvu zote kitendo hiki, ni kitendo ambacho hakikubaliki hata kidogo"

"Ndugu zangu wana Shabaka, najua na nyie hiki kitendo hamkikubali, waliokifanya kitendo hiki hawako mbali na sisi na kila mtu kwenye moyo wake, anahisi kwamba kuna mtu Fulani, ndio aliehusika, kwa sababu mtoto amechinjwa kabisa, nimemuona hapo, ninyi ndio wenyeji wa maeneo haya, tunaomba ushirikiano wenu, ili hawa waliohusika na kitendo hiki cha kinyama wapatikane wafikishwe mbele ya Sheria",   alisema William

Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Geita Last Lingson anasema baadhi vitendo vya ukatili kwa Watoto vinatokana na visasi kwa wazazi pamoja na Imani za kishirikina ambazo zimeendekezwa kwenye jamii kwa kukosa Elimu ya hofu ya Mungu na utu kwenye familia na nyumba za Ibada.

Jeshi la Polisi mkoa wa Geita bado linaendelea na uchunguzi ili kujua nani aliyehusika na tukio hilo ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya dola