Jumatano , 23rd Nov , 2022

Serikali Mkoani Geita imewataka viongozi wa jumuiya za maji kuacha ubadhilifu wa fedha wanazokusanya kwenye uuzaji wa maji badala yake wawe waadilifu kwenye ukusanyaji na matumizi sahihi ili kila mwananchi aweze kunufaika na uwepo wa miradi ya maji kwenye eneo lake.

Mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo

Maagizo hayo yametolewa na mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo wakati anafungua mafunzo kwa viongozi wa jumuiya hizo wilayani humo baada ya kuonekana baadhi yao kutumia fedha hizo kwa matumizi yasiyo ya huduma za Maji.

"Haipendezi kwamba sisi ambao ni viongozi wajumbe wa bodi wajumbe wa kamati ya vyombo hivi, tukaonekana tena tumekuwa tena shida ya fedha ambazo zinakusanywa, zinapatikana baada ya kuuza Maji katika Miradi yetu, twende tukafanye uadilifu mkubwa lakini pia tukaoneshe utendaji mwema  kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu", amesema Wilson Shimo. 

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Geita  Mhandisi Sunday Charles amesema lengo la mafunzo hayo ni kuvijengea uwezo vyombo vinavyosimamia huduma za Maji vijijini ili viweze kusimamia miradi ya Maji iwe bora na endelevu.

"Fedha zinazokunywa, sisi Ruwasa tukishaweka miundombinu sehemu nyingine sasa ziandaliwe zifikishiwe huduma sio tu Ruwasa ilipoishia hapohapo mradi uishie naona sehemu jingine sana zimeshaanza kupanuliwa ukienda Lwamgasa kule tumeshaunganisha zaidi ya watu 100, vevile Nyakagwe tumeunganisha watu wengi sana, kwahiyo na sisi tunakuwa tuna washauri mara kwa mara fedha hizi mlizokusanya sio tu fahari kuwa nazo kwenye account, zichukuliwe fedha hizo zipeleke huduma sehemu ambazo hatukuzifikia", amesema Charles. 

Baadhi ya viongozi wa jumuiya hizo wameishikuru serikali kwa kuendelea kupeleka miradi ya Maji vijijini.
"Hapa tulipo tumefanya huduma ambayo, tumepata huduma ambayo huwa inatusaidia sana hatufati Maji kwenye umbali mrefu alafu, wanazidi kutupa mafunzo Ruwasa wilaya ya kuboresha miradi yetu, kwanza tunefundishwa mafunzo ya control number ambayo itakusanya fedha kwa wakati mmoja mwisho wa siku tutaendelea kuboresha miradi katika CBWSo zetu", amesema Maige.