Jumanne , 27th Mei , 2025

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, kwa mamlaka aliyonayo ameamua kusitisha kuwapa ruzuku CHADEMA hadi watakapotekeleza maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa sababu chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewakumbusha wanachama na viongozi wa CHADEMA kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Msajili anayo mamlaka ya kusimamisha usajili wa chama hicho, endapo kitaendelea kuwatambua wanachama waliotajwa kuwa ni viongozi wa chama hicho.

Aidha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesisitiza kuwa John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahim Juma, Godbless Lema, Dkt. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu na Hafidhi Ali Salehe sio viongozi wa CHADEMA pamoja na watendaji wengine wote walioteuliwa katika kikao cha Baraza Kuu la Januari 2025.

Msajili huyo pia amebainisha kwamba endapo CHADEMA wataendelea kukaidi kutekeleza maamuzi na maelekezo waliyopatiwa basi mamlaka husika zitatakiwa kuchukua hatua za kisheria na kijinai pamoja na kuwasimamisha wanaojifanya kuwa viongozi wa CHADEMA katika kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa kifungu cha 21E cha sheria ya vyama vya siasa nchini.