Jumapili , 17th Aug , 2025

Watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 16, 2025, katika Ukumbi wa Mwitongo, Kata ya Mailimoja, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu kumi, wakiwemo wanawake watatu, kwa tuhuma za kukusanyika na kupanga njama za kufanya uhalifu.

Watuhumiwa hao walikamatwa jana Agosti 16, 2025, katika Ukumbi wa Mwitongo, Kata ya Mailimoja, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamanda Salim Morcase, Agosti 17/2025 amethibitisha kukamatwa kwa watu hao. Alieleza kuwa Polisi walipata taarifa kutoka kwa wasiri wao kuhusu uwepo wa kundi hilo katika ukumbi huo, likidaiwa kuwa wanajihusisha na kupanga vitendo vya uhalifu.

Kamanda Morcase amewataja watuhumiwa waliokamatwa na maeneo wanayoishi kuwa ni Focus Kasaka (Mwanza), Harouna Zangina (Goba, Dar es Salaam),Abdallah Mazengo (Mwanana, Arusha), Samson Rabani (Tangini, Kibaha) na Pendo Mwasomola (Nzovwe, Mbeya). Wengine ni Mkombozi Hatibu (Mailimoja, Kibaha) ,Mzambia Kabuje (Kijenge, Arusha), Furaha Mbise (Ubungo, Dar es Salaam) ,Upendo Msechu (KCMC, Moshi) na Upendo Mwalushwa (Mbezi, Dar es Salaam).

Aidha, Kamanda Morcase amebainisha kuwa jeshi hilo linaendelea kuwahoji  watuhumiwa hao na baada ya upelelezi kukamilika, hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.