Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman amesema kuwa Kiongozi wa zamani wa Kundi la Al Quaeda, Osama Bin Laden aliwatumia watu wa Saudi Arabia kuharibu uhusiano wao na Marekani baada ya ziara yake nchini Marekani kuibua hasira ya manusura wa wa tukio la tarehe 11 mwezi Septemba 2001.
Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa Habari baada ya kutembelea Washington, DC, Salman alisema anahuzunishwa na tukio hilo lakini kinachomuumiza zaidi ni kitendo cha watu wa Saudia kutumika kutekeleza mauaji hayo ili kuharibu uhusiano wa mataifa hayo mawili.
"Osama bin Laden alitumia watu wa Saudi katika tukio hilo kwa lengo moja kuu: kuharibu uhusiano huu, kuharibu uhusiano wa Marekani na Saudi," alisema.
"Kwa hivyo yeyote anayekubaliana na mtazamo huo inamaanisha anasaidia madhumuni ya Osama bin Laden ya kuharibu uhusiano huu". Aliongeza.
Mashambulizi ya Septemba 11 yalikuwa mfululizo wa mashambulizi manne ya kigaidi yaliyoratibiwa na kundi la kigaidi la Kiislamu la al-Qaeda nchini Marekani asubuhi ya Jumanne, Septemba 11, 2001. Mashambulizi hayo yaliua watu 2,997, kujeruhi zaidi ya wengine 6,000.
