Alhamisi , 18th Dec , 2025

Akikabidhi cheti hicho kwa niaba ya kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro afisa Mnadhimu wa jeshi la Polisi mkoa Kamishna Msaidizi Abel Mtagwa, amekipongeza kituo hicho kwa mchango wake mkubwa katika kuripoti taarifa sahihi kuhusu usalama barabarani.

Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro, kimekabidhi cheti cha pongezi kwa kituo cha East Africa Tv na Radio kwa mchango wake wa kutoka elimu ya usalama barabarani kupitia habari na vipindi vya elimu kwa umma. 

Cheti cha pongezi kimetolewa kwa kituo hicho kupitia mafunzo ya kujengeana uwezo yaliyowashirikisha watangazaji na askari polisi wanaoshiriki kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia radio na televisheni mkoani Kilimanjaro. 

Akikabidhi cheti hicho kwa niaba ya kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro afisa Mnadhimu wa jeshi la Polisi mkoa Kamishna Msaidizi Abel Mtagwa, amekipongeza kituo hicho kwa mchango wake mkubwa katika kuripoti taarifa sahihi kuhusu usalama barabarani.

Vile vile ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa  wanahabari kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha jamii inakuwa salama kwa kufuata sheria za usalama barabarani .

Tukio hilo la ugawaji wa vyeti imeenda sambamba na semina maalumu kwa watangazaji wa redio na television wa vipindi vya usalama barabarani iliyolenga kuwajengea uwezo wa kuripoti matukio mbalimbali ya usalama barabarani kupunguza ajali za barabarani. 

Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nassoro Sisiwayah amesema katika kipindi hiki cha  kuelekea  mwisho wa mwaka mkoa huo umekuwa ukipokea wageni wengi ambapo ameweka wazi kuwa Polisi itahakikisha usalama unaimarika kipindi watakapo kuwepo ndani ya mkoa huo.

Aidha amewataka wageni wote wanaingia ndani ya mkoa huo kuzingatia sheria za usalama barabarani zilizowekwa ili kuhakikisha wanafurahia sikukuu hizo katika hali ya usalama, amani na utulivu .

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafirishaji Ardhini(LATRA) mkoa wa Kilimanjaro Paul Nyello, ameahidi ushirikiano zaidi na vyombo vya habari pamoja na wadau wa usalama barabarani katika kuthibiti vitendo vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani. 

Naye Mkaguzi wa Polisi Allen Chittunda toka Dawati la elimu ya Usalama Barabarani mkoani humo aliwakumbusha wanahabari kujua namna bora ya kuripoti matukio ya ajali ili kuondoa taharuki kwa wananchi, kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinakuwa sahihi kwa kuzingatia weledi wa kazi yao. 

Semina hiyo ya siku moja iliyowezeshwa na mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini (LATRA), imeratibiwa na jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni mwendelezo wa mikakati inayolenga kuimarisha mahusiano na uwezo wa kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia vyombo vya habari vya utangazaji mkoani Kilimanjaro.