Friday , 14th Dec , 2018

Waziri wa Nishati, Dk.Medard Kalemani amemsimamisha kazi Mhandisi Faustina Tuya na Mtaalamu Msaidizi wa Ushauri na ufundi, Gady Eliya katika mradi wa uwekaji umeme vijijini Rea katika kijiji cha Kimnyaki Wilayani Arumeru.

Waziri wa Nishati, Dk.Medard Kalemani.

Akizungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi olimringaringa Kata ya Kimnyaki Wilayani humo, Dk. Kalemani aliagiza wataalam hao wawili waondoke mara moja katika kumsaidia mkandarasi wa kampuni ya Nipo Group kwa sababu wameshindwa kwenda na kasi ya mradi.

Sitaki kuwaona hawa watu wawili waondoke kuanzia leo na kesho waje wengine kusaidiana na huyu mkandarasi, sababu ninachotaka wananchi wapate umeme kwa wakati, haiwezekani miezi minne tangu mradi wa Rea awamu ya tatu uanze lakini hadi leo vijiji viwili kati ya 13 ndivyo vimewekewa  umeme,” amesema.

Pia alimwagiza mkandarasi wa kampuni ya Nipo Group anayetekeleza mradi huo katika Wilaya ya Longido na Arumeru, ambako kote alifanya ziara ya kukagua miradi, kuhakikisha ndani ya siku kumi anaunganisha umeme kwenye vijiji kumi vya kila Wilaya hizo, vinginevyo naye atatumbuliwa.

Dk. Kaleman alimwagiza Meneja wa Tanesco Wilaya ya Arumeru  na wa Wilaya ya Longido, kumfuatilia mkandarasi huyo ili akishindwa ndani ya siku hizo alizotoa kutimiza agizo hilo apewe barua ya kusitisha mkataba aliopewa.

Alisema kazi hiyo wamepewa wakandarasi wazawa ili kuwapima kama wanaweza kuendana na kasi ya Rais John Magufuli na endapo watashindwa kazi hizo zitafanywa na Shirika la Umeme la Tanesco kwa sababu wanao uwezo.