Thursday , 27th Oct , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea ujumbe kutoka kwa mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Mohamed Al Suwaidi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam

Ujumbe huo umewasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi Bw. Mohamed Al Suwaidi aliyekutana baye na kufanya mazungumzo na rais Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika ujumbe huo Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan amemuahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo imedhamiria kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan

 

Mfuko wa maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na katika mazungumzo ya leo Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo ameonesha nia ya kushirikiana zaidi na Tanzania katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, usafiri wa anga na madini.

Pamoja kumshukuru Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi na Kaimu Rais Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais Magufuli ameialika nchi hiyo kupitia mfuko wake wa Maendeleo na wadau wengine wa maendeleo kuja kuwekeza hapa nchini katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa bandari, ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kati ambayo itazinufaisha nchi nyingine saba za Afrika Mashariki na kati ambazo hazina bandari.