Tuesday , 31st Jan , 2017

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bw. Akinwumi Adesina amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli, huku akiahidi kuwa benki hiyo itaizalishia Tanzania umeme wa gharama nafuu.

Mazungumzo hayo yamefanyika nchini Ethiopia,ambako Rais Magufuli amehudhuria mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi za Afrika ambapo amemshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka Benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Pia Rais Magufuli amemuomba Rais huyo wa AfDB kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano huo hasa katika maeneo ya kipaumbele ambayo Tanzania inayatekeleza hivi sasa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina mara baada ya kumaliza mazungumzo yao mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kwa upande wake Bw. Akinwumi Adesina amesema Benki hiyoitaendeleza ushirikiano na uhusiano wake na Tanzania na kwamba Tanzania itanufaika kupitia vipaumbele vipya vya AfDB viitwavyo “Hi 5” vinavyohusisha uwezeshaji miradi ya uzalishaji wa nishati, ujenzi wa viwanda, uzalishaji wa chakula, miundombinu ya kuunganisha nchi na nchi na kuboresha maisha ya watu.

Pia Bw. Akinwumi Adesina amekubali ombi la Mhe. Rais Magufuli la kuitaka AfDB kushirikiana na Tanzania kupata suluhisho la kuzalisha umeme mwingi na wa gharama nafuu na ameahidi kumtuma Makamu wa Rais wa AfDB anayeshughulikia masuala ya nishati kuja Tanzania haraka iwezekanavyo ili kuanza utekelezaji wa ombi hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn wakati akitoka kwenye mkutano wa AU mjini Addis Ababa nchini Ethiopia

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Hailemariam Desalegn na amemualika kufanya ziara rasmi nchini Tanzania ili wapate nafasi ya kuzungumza zaidi juu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo.

Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli, Mhe. Hailemariam Desalegn amempongeza kwa mabadiliko makubwa ya uchumi ambayo Serikali ya awamu ya tano inayafanya nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kukabiliana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Rais Magufuli na Rais Jacob Zuma

Vilevile Rais Magufuli amekutana na Rais wa Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Zuma ambapo pamoja na kukubali kufanya ziara rasmi nchini Tanzania, viongozi hao wamekubaliana kuwa baada ya kazi kubwa ya harakati za ukombozi nchi hizi sasa zina kila sababu ya kuelekeza nguvu katika kuongeza biashara na uwekezeji.

Picha ya pamoja ya wakuu wa nchi za Afrika

Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambao Rais Magufuli amehudhuria kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani umemalizika leo Mjini Addis Ababa na Mhe. Rais Magufuli anatarajiwa kurejea nyumbani kesho