Mabasi hayo, maarufu kama ‘school bus’, ambayo yamebainika kuwa hayana sifa, ni sawa na asilimia 64.3. Hadi sasa yanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kubainika kuwa yana makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ubovu.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Awadhi Haji, alisema hadi juzi walikuwa wamefanya ukaguzi wa magari 185 na 119 kati ya hayo, yamebainika kuwa na makosa mbalimbali.
“Tunafanya ukaguzi wa ‘school bus’ kwa lengo la kuona ubora ili tujue kama yanakidhi viwango vya sheria za usalama barabarani. Hadi sasa tumekagua magari 185 kwa Mkoa wa Dar es Salaam 119 tumeyakuta yana upungufu mwingi ikiwamo ubovu wa bodi, matairi chakavu na viti vibovu,” alisema.