Tuesday , 23rd Sep , 2014

Aliyekuwa mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Tanzania, Askofu Valentino Mokiwa, ameonya juu ya kuongezeka kwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, ambapo amefananisha tatizo hilo kuwa ni sawa na bomu linalosubiri kufyatuka wakati wowote.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa.

Huku akiweka bayana kuwa yeye mwenyewe hayupo tayari kushuhudia bomu hilo likifyatuka, askofu Mokiwa pia amezungumzia mchakato wa katiba na kufafanua kuwa vikao vya bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma kimaadili na kwa mtazamo wa Watanzania wengi likiwemo Jukwa la Kikristo ni batili.

Askofu Mokiwa amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuzungumza na waumini wa dini mbali mbali nchini, ambao wanaunda baraza la kitaifa la kiimani linalounganisha waumini hao kama njia ya kuimarisha amani pamoja na uvumilivu wa kiimani baina yao.

Wakati huo huo, wajasariamali nchini Tanzania wameombwa kushirikiana bila kujali itikadi zao za kidini ili kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri fedha wanazokusanya ili ziwasaidie kutoka daraja moja la kimaisha hadi lingine.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salim, ametoa wito huo wakati wa maonyesho ya wajasiriamali kutoka taasisi mbalimbali za kidini nchini, ambapo amesema wajasiriamali wa ndani wana umuhimu mkubwa katika jamii na ni vyema serikali kuwasaidia katika kujitangaza kwenye masoko ya nje.

Kwa upande wao wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo akiwemo Vailet Msuya amewataka wajasiriamali wakubwa kushirikiana nao haswa katika kununua bidhaa zao na sio kuiga ubunifu wao, jambo ambalo linazorotesha soko la bidhaa zao.