
Mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani (FAO) Jose Graziano Da Silva
Bw. Da SIlva ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya chakula duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 16, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu inasema "Hali ya hewa inabadilika, chakula na kilimo pia", hivyo ametoa wito kwa nchi kujumuisha masuala ya chakula na kilimo katika mipango ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameongeza kuwa uwekezaji hasa katika maeneo ya vijijini ni muhimu sana ili kuhakikisha uhakika wa chakula, na kuongeza kuwa chakula ni haki ya msingi ya binadamu, lakini bado kuna watu karibu milioni 800 wanakabiliwa na njaa duniani kote.
Pia Bw. Da Silva amesema kuwa bila uhakika wa chakula na lishe ya kutosha kwa wote, malengo ya maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa, ndiyo maana ajenda ya mwaka 2030 inatoa wito wa kutokomeza njaa pamoja na kuchagiza kilimo endelevu.
Hata hivyo ameonya kuwa malengo hayo ni bayana yako hatarini wakati mabadiliko ya hali ya hewa yakiendelea, tayari yanaathiri rutuba kwenye udongo, misitu, bahari, maeneo ambayo ni tegemeo kwa sekta ya kilimo na uhakika wa chakula.