Wednesday , 27th Jan , 2016

Mbunge wa Tarime vijijini kupitia chama cha CHADEMA Joh Heche, amesema kitendo cha kutorushwa live kwa matangazo ya bunge ni kuvunja katiba na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kama inavyoelezwa kwenye katiba ya nchi.

John Heche ameyasema hayo leo alipokuwa akiomba muongozo kwa mwenyekiti wa bunge Mh. Andrew Chenge, baada ya kutolewa taarifa kutoka kwenye kikao cha kamati ya uongozi, kilichokuwa kinajadili hoja ya kupinga taarifa iliyotolewa na waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Mh. Nape Nnauye, kuhusu kutorushwa moja kwa moja matangazo ya bunge kwenye televisheni ya taifa, ili kubana matumizi ya fedha za uma.

“ Kwa mujibu wa katiba inasema kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati mbali mbali, tuko hapa kujadili masuala muhimu ya jamii yetu, tutakuwa wa ajabu kukubali kuvunja katiba kuzuia wananchi kupata taarifa inayohusu bunge lao na maisha yao”, alisema John Heche.

Pamoja na hayo mbunge huyo ameomba kupewa mchanganuo wa gharama ambazo Mh. Nape Nnauye amezitaja kuwa ni kubwa, pale matangazo hayo yanaporushwa.

“Sasa mwenyekiti Mh. Nape atueleze tujue hizo gharama anazozisema Nape zimetoka wapi?', alisema John heche.

Mwenyekiti wa bunge alisema suala hilo litatolewa ufafanuzi baadae na kuwataka wabunge kuendelea na na ratiba ilivyopangwa ya kujadili hotuba ya rais.