Monday , 9th Mar , 2015

Taasisi ya Shirika la kijamii Tanzania Women of Achievement Awards (TWAA), wamewatunukia tuzo Wanawake mbali mbali Nchini kwa mafanikio yao katika tuzo za Wanawake wenye MafanikioTanzania zilizofanyika Machi 7, katika Hoteli ya Serena

jijini Dar es Salaam, ambazo mwaka huu zinafanyika kwa mwaka wa Saba, mfululizo tangu kuanzishwa kwake, likiwa na lengo la kuwatambua na kuwapongeza wanawake ambao wamechangia maendeleo Tanzania katika nyanja tofauti.

Katika tuzo, Rais wa TWAA, Irene Kiwia aliweza kumtangaza Mwanamke aliefanya vizuri ndani ya Mwaka mzima‘Woman of the Year’, ambapo tuzo hiyo ilienda kwa Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia, Mkoa wa Kinondoni, Inspekta Prisca Komba.

Mbali na tuzo hiyo, kwa upande wa tuzo ya mwanamke aliefanya vizuri katika maisha yake ‘Lifetime Achievement Award’, ilienda kwa Mama Debora Mwenda ambaye kitaaluma alikuwa mwandishi wa habari na mcheza michezo ya kuigiza miaka ya zamani, kupitia Redio Tanzania, (RTD), wakati huo

Kwa upande wake, Rais TWAA, Bi. Irene Kiwia alipongeza wadau mbalimbali waliojitokeza kusaidia tuzo hizo. “Lengo la TWAA ni kusheherekea mafanikio ya wanawake hawa na kazi wanazozifanya kwenye jamii kupitia nyanja tofauti ndani ya Tanzania. Washindi waliopatikana ni kuzingatia vigezo mbalimbali vilitumika katika kuwachagua kama vile utofauti waliouonyesha katika jamii zao, jinsi gani wameweza kuwavutia na kuwashawahi watu wengine, na jinsi gani wameweza kuwagusa na kuwafikia watu tofauti tofauti.” Alieleza.

Aidha, alimwelezea, Inspekta Prisca Komba kuwa ni mwanamama wa kuigwa kwani ameweza kufanikisha uwepo wa dawati la Jinsia na namna anavyowashughulikia masuala ya wanawake katika vituo vya Polisi, kesi zinazowahusu, ambapo hali hiyo awali haikuwapo hapa Nchini kutokana na jamii nyingi hasa jeshi la Polisi ikiwemo kwa wanawake wengi kukosa fursa na haki zao za msingi hasa katika madawati ya mashitaka ya jeshi la Polisi.

Bi. Kiwia alisema kwamba “ Tuzo hizo zitakuwa zinaenda sambamba na na mafunzo ya kujenga uwezo wa wasichana viongozi katika nyanja tofauti walio kati ya umri wa miaka 18-27 kutoka mikoa yote ya Tanzania ambayo yatachukua wiki 6.

Wasichana hao watakutanishwa na wanawake wanaofanya vizuri katika biashara, kazi za jamii na idara tofauti kwa ajili ya kupewa motisha na kujifunza. Huku mategemeo yakiwa ni kuwa baada ya mafunzo hayo wasichana wataenda kuwa chachu ya mabadiliko mikoani kwao na kuwafundisha wenzao wengi ili kusambaza mori wa maendeleo na mabadiliko kwa wasichana wadogo nchini kote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWAA, Bi. Sadaka Gandhi alisema “suala la uwezeshaji kwa wanawake linapewa kipaumbele duniani kote, tuzo hizi zitaonyesha uwezo na ugunduzi wa wanawake katika sehemu tofauti. Tunaamini kuwa wale wote walioshinda leo watakuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana kutoka vijijijini, wafanyabiashara na wanawake wengi chini Tanzania”.alisema Bi. Gandi.

Aidha, tuzo zingine walizochukua wanawake hao ni pamoja na Sanaa na utamaduni, ujasiriamali, elimu, afya, sayansi na teknolojia, kilimo, ustawi wa jamii, michezo, umma, mshiriki wa mafanikio mwenye umri mdogo, mwanamke aliefanya vizuri ndani ya mwaka mzima na mwanamke aliefanya vizuri katika maisha yake.

Aidha, tuzo hizo kwa mwaka huu zilikuwa chini ya Kamati ya TWAA ikijumuisha Bi Mary Rusimbi – Mwanaharakati na Mwanzilishi wa Programu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania, Jaji Joaquine De Mello, Dk. Marcelina Chijoriga – kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bwana.

Wengine ni Innocent Mungy – Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Sadaka Gandi – Mwanasaikolojia na mfanyakazi za Jamii, Irene Kiwia – Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya mahusiano ya jamii Frontline Porter Novelli.