Tuesday , 18th Oct , 2016

Aliyewahi kuwa Katibu wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Samweli Kasori, ametoa wito kwa serikali kuwekeza nguvu zaidi katika sekta ya elimu kwa kuwa hiyo ndiyo ufunguo wa maisha na maendeleo ya nchi.

Aliyewahi kuwa Katibu wa Baba wa Taifa, Mzee Samweli Kasori.

Mzee Kasori ametoa ushauri huo baada ya kutembelea Shule ya Sekondari Nsibugani iliyopo Mkoani Pwani kwa lengo la kushuhudia vijana wasomi na wazalendo waliojitolea kufyatua matofali elfu 45 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu katika shule hiyo.

Akizungumza katika kikao kilichowahusisha vijana hao baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya shule hiyo Mzee Kasori amesema elimu ndiyo njia muhimu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jamii pamoja na kupambana na umasikini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuruanga Filbeto Sanga, ametoa wito kwa wananchi hususani vijana kuendelea kuwa na moyo wa uzalendo na kujitolea ili kufanikisha malengo mbalimbali ya maendeleo.